Dodoma FM

Uchaguzi wa viongozi soko la Machinga waamsha matumaini kwa wafanyabiashara

12 January 2026, 3:13 pm

Picha ni baadhi ya wafanyabiashara katika soko la wazi la Machinga Complex jijini Dodoma. Picha na Dodoma FM.

Kufuatia kukamilika kwa zoezi la uandikishaji kuelekea uchaguzi wa viongozi wa soko hilo wafanyabiashara soko la wazi la Machinga Complex wamesema matarajio yao ni kuwa na viongozi wawajbikaji.

Na Mariam Kasawa.

Wafanyabiashara wa Soko la Wazi la Machinga wameeleza matumaini na matarajio makubwa kufuatia kukamilika kwa zoezi la uandikishaji kuelekea uchaguzi wa viongozi wa soko hilo.

Hayo waliyasema baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki katika zoezi hilo la uandikishaji mbele ya waandishi wa habari waliofika sokoni hapo kupata maoni yao juu ya mwenendo mzima wa mchakato wa uchaguzi huo.

Nae, Mfanyabiashara wa Soko la Wazi la Machinga, Habiba Kibiriti amesema kuwa matarajio yao ni kuwachagua viongozi ambao watatumikia vyeo vyao kwa uadilifu na kusimamia maslahi ya wafanyabiashara. “Matarajio yetu makubwa ni kuchagua viongozi ambao wataweza kusimamia maslai yetu bila upendeleo lakini pia kiongozi ambae ataweza kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa michango na tozo mbalimbali ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima” alisema Kibiriti.

Picha ni baadhi ya wafanyabiashara katika soko la wazi la Machinga Complex jijini Dodoma. Picha na Sauti Yetu.

Kwa upande wake, mfanyabiashara Shafu Hassan ametoa wito kwa viongozi ambao watapata nafasi ya kusimamia soko hilo. “Nipende kutoa wito wangu kwa viongozi ambao watapata nafasi ya kutusimamia wafanyabiashara ni kwamba washirikiane kwa karibu na mamlaka za serikali ili kuhakikisha soko linazidi kukua” alitoa wito Hassan.

Nae Menejawa Soko la Wazi la Machinga, CPA. Jonhstone Kahungu, amesema kuwa kupitia uchaguzi huo, wafanyabiashara wana imani kubwa kwa viongozi watakao wachagua. “Mwamko wa kuwapigia kura viongozi wa Soko la Wazi la Machinga kwa wafanyabiashara ni wa hali ya juu kwasababu kupitia uchaguzi huu imani yao ni kusikilizwa na kutatuliwa kero zao. Hivyo niwasihi wafanyabiashara kuwa wajitokeze kupiga kura ili kupata kiongozi bora na atakayeweza kutatua changamoto zao” alisema CPA. Kahungu.