Dodoma FM

Tume ya utumishi wa umma yafafanua rufaa, malalamiko ya watumishi

23 December 2025, 5:04 pm

Picha ni Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma.Picha na Anwary Shaban.

Watumishi kupinga kutokulipwa stahili zao na waajiri, ikiwemo mishahara, stahili za uhamisho pamoja na posho mbalimbali za kisheria zinazotokana na utekelezaji wa majukumu yao.

Na Anwary Shaban.

Tume ya Utumishi wa Umma imetoa ufafanuzi kuhusu rufaa na malalamiko yaliyowasilishwa na watumishi wa umma mbele yake, ambapo jumla ya rufaa na malalamiko 88 yalipokelewa na kuamuliwa na tume.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso, amesema kuwa katika rufaa zilizowasilishwa na kuamuliwa, makosa yaliyobainika mara kwa mara ni pamoja na utoro kazini, kutotekeleza majukumu ipasavyo, na ukiukaji wa taratibu za utumishi wa umma.

Sauti ya John Mbisso.

Kwa upande wa malalamiko, Mbisso ameeleza kuwa mengi yalihusu watumishi kupinga kutokulipwa stahili zao na waajiri, ikiwemo mishahara, stahili za uhamisho pamoja na posho mbalimbali za kisheria zinazotokana na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Aidha, katika kutekeleza jukumu la urekebu na usimamizi wa utumishi wa umma, tume ilifanya ziara za kikazi katika taasisi tano za serikali zilizopo Manispaa ya Morogoro, zikiwemo Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Sauti ya John Mbisso.

Mbisso amesisitiza kuwa Tume ya Utumishi wa Umma itaendelea kutoa wito na kuwakumbusha watumishi wa umma, waajiri, mamlaka za ajira pamoja na mamlaka za nidhamu kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na maadili ya kazi ili kuepusha migogoro na malalamiko yasiyo ya lazima.

Sauti ya John Mbisso.