Dodoma FM
Dodoma FM
19 December 2025, 5:46 pm

Amesema muongozo huo utakuwa chachu muhimu katika kukuza biashara changa, ndogo na za kati.
Na Mariam Matundu.
Serikali imezindua Mfumo wa Muongozo wa Kitaifa wa Vituo vya Uendelezaji Biashara, hatua inayolenga kuimarisha mazingira ya biashara ndogo na za kati pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. James Henry Kilabuko, amesema muongozo huo utakuwa chachu muhimu katika kukuza biashara changa, ndogo na za kati, na kuwawezesha wafanyabiashara kuhimili ushindani wa ndani na nje ya nchi.
Dkt. Kilabuko ametoa wito kwa watoa huduma za uendelezaji biashara nchini kuhakikisha wanatumia muongozo huo kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara, hususan wale waliopo pembezoni mwa miji na vijijini, ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo ya kiuchumi.
Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), CPA Beng’i Issa, amesema uzinduzi wa muongozo huo ni hatua muhimu kwa Serikali katika kuboresha mazingira ya ujasiriamali, kukuza biashara ndogo na za kati, na kuchochea maendeleo jumuishi na endelevu kwa wananchi.