Dodoma FM

Wanawake watakiwa kueleza changamoto michakato ya kupata mkopo

18 December 2025, 3:53 pm

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa ziara yake ya kutembelea na kufuatilia utekelezaji wa programu za uwezeshaji wanawake kiuchumi.Picha na Maendeleo ya jamii.

Wanawake wa Jukwaa walioshiriki katika kikao hicho wamemshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa kuwapa nafasi ya kusikilizwa.

Na Mariam Matundu.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wanawake katika vikundi mbalimbali kueleza changamoto walizokumbana nazo katika mchakato wa kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, ili changamoto hizo ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Dkt. Gwajima ametoa wito huo Desemba 17, 2025 wakati wa ziara yake ya kutembelea na kufuatilia utekelezaji wa programu za uwezeshaji wanawake kiuchumi.

‎Katika ziara hiyo, Waziri Dkt. Gwajima ametembelea vikundi vya wanawake wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi.

Aidha, amefanya kikao na Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi la Wilaya hiyo, ambapo amebaini kuwa baadhi ya wanawake wanakumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa ujuzi wa kuandaa maandiko ya miradi, kushindwa kutimiza baadhi ya vigezo kama vile kutokuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA), pamoja na changamoto nyingine zinazowafanya washindwe kunufaika na mikopo hiyo.

Waziri‎ Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali, imeweka mikakati madhubuti ya kuwasaidia wanawake kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika upatikanaji wa mikopo ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa miradi, kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi.

Sauti ya Dkt. Gwajima.

‎Wanawake wa Jukwaa walioshiriki katika kikao hicho wamemshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa kuwapa nafasi ya kusikilizwa na kueleza changamoto wanazokumbana nazo katika mchakato wa kupata mikopo ya Serikali.

Wamesema hatua hiyo imewapa matumaini mapya, na wameahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali na viongozi husika ili kuhakikisha changamoto zilizobainishwa zinapatiwa ufumbuzi na wanawake wengi zaidi wanapata fursa za uwezeshaji wa kiuchumi.