Dodoma FM
Dodoma FM
11 December 2025, 3:27 pm

Picha ni Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Mazengo , Rehema Nkungu katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi. Picha na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi hiyo imefanywa na Kamati ya Uongozi wa Mtaa wa Kigamboni pamoja na uongozi wa shule hiyo ili kujionea namna shughuli zinavyotekelezwa.
Na Lilian Leopold.
Serikali kupitia mradi wa BOOST kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais- Tamisemi imetoa zaidi ya shilingi milioni 267 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa,ujenzi wa matundu ya vyoo na ujenzi wa kituo cha utafiti kwa walimu katika shule ya Msingi Mazengo iliyopo kata ya Kikuyu Kaskazini jijini Dodoma, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Mtendaji wa mtaa wa Kigamboni Farijala Kunga amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa shuleni hapo inazingatia ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Mazengo , Rehema Nkungu amesema uchakavu wa miundombinu ya madarasa na kuvuja kwa paa nyakati za mvua kumeathiri ufundishaji na kusababisha utoro kwa wananfunzi lakini kupatikana kwa madarasa mapya kutaboresha taaluma na kupunguza utoro mkubwa uliokuwepo.

Picha ni Mwenyekiti wa mtaa wa Kigamboni Mathayo Ng’okorome katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi. Picha na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Kigamboni Mathayo Ng’okorome ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu na kuongeza kuwa ziara hiyo imeratibiwa kwa ushirikiano wa kamati ya uongozi wa mtaa ili kuimarisha uhusiano kati ya serikali ya mtaa, walimu na jamii.
Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 inaonyesha utekelezaji wa ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi kwa njia ya kuongezeka kwa vyumba vya madarasa na miundombinu ya msaada ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.