Dodoma FM
Dodoma FM
2 December 2025, 4:29 pm

Kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ya jiji la Dodoma, serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo kujenga matundu ya vyoo, madarasa na maabara, lengo ni kuwapatia wanafunzi mazingira salama wezeshi ya kujifunzia.
Na Lilian Leopold.
Timu ya Menejimenti ya halmashauri ya jiji la Dodoma imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika shule mbalimbali ikiwemo shule ya sekondari Hazina, shule ya sekondari Makole, shule ya msingi Msalato Bwawani, shule ya msingi Chihoni na shule ya msingi Mbawala.
Lengo la ziara hiyo ni kuhamasisha umalizaji wa miradi hiyo kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mikataba ya ujenzi.
Katika ziara hiyo, timu ilikagua ujenzi wa madarasa pamoja na matundu ya vyoo katika shule hizo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo,Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Francisca Mselemu amesema serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira rafiki na bora ya kujifunzia.

Kwa upande wao, baadhi ya walimu wakuu kutoka shule ya sekondari Hazina, Makole na shule ya msingi Msalato Bwawani wamesoma taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo na kueleza hatua zilizofikiwa.
Naye Mchumi kutoka halmashauri ya jiji la Dodoma Harold Jeremia amewapongeza walimu kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa madarasa katika shule hizo.