Dodoma FM
Dodoma FM
1 December 2025, 5:20 pm

Maeneo mengi katika Mkoa wa Dodoma na wilaya zake ikiwemo Dodoma, Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Chamwino, Chemba na Kondoa yanatarajiwa kupata mvua chache hadi za wastani katika kipindi chote cha msimu.
Na Mwandishi wetu.
Wananchi wameendelea kupata elimu kuhusu uchaguzi sahihi wa mazao ya kupanda, huku msimu wa kilimo ukitarajiwa kuanza hivi karibuni kufuatia mvua zinazotarajiwa kunyesha mwanzoni mwa mwezi Desemba.
Hayo yameelezwa na Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Agnes Woisso wakati akitoa elimu juu ya utabiri huo kwa wakazi na wakulima wa kata ya Hombolo Bwawani.
Bi. Agness amewahimiza wakulima kulima kitaalam msimu huu kutokana na kiwango kidogo cha mvua kinachotarajiwa, tofauti na miaka iliyopita. Aidha, wameelekezwa kupanda mazao yanayostahimili upungufu wa mvua kama vile mihogo, mtama, uwele na njugumawe kwa ajili ya chakula, pamoja na mazao ya biashara kama karanga, alizeti na zabibu ili kujihakikishia kipato na usalama wa chakula.

Kwa upande mwingine, Afisa Kilimo wa Kata ya Hombolo Bwanani, Allen Katambala amesema kuwa kwa sasa wakulima wanapaswa kufuata ushauri wa wataalam ili waweze kufanya kilimo chenye tija na akawaasa wakulima juu ya matumizi bora ya mbegu.
Kulingana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania maeneo mengi katika Mkoa wa Dodoma na wilaya zake ikiwemo Dodoma, Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Chamwino, Chemba, na Kondoa yanatarajiwa kupata mvua chache hadi za wastani katika kipindi chote cha msimu. Huku kiwango cha mvua kinavyotarajiwa kikiwa kati ya milimita 590-670 katika wilaya tofauti ikilinganishwa na wastaniwa miaka 30 kwa mkoa huu.