Dodoma FM

Familia ya MC Pilipili yathibitisha mwili wake kukutwa na majeraha

17 November 2025, 3:22 pm

Picha ni mchekeshaji na mshereheshaji maarufu nchini, Emmanuel Mathias maarufu kama MC Pilipili.Picha na Dodoma fm.

Familia haikupata nafasi ya kuuona mwili mara moja baada ya taarifa za kifo kutokana na majukumu waliyokuwa nayo.

Na Seleman Kodima.
Familia ya marehemu mchekeshaji na mshereheshaji maarufu nchini, Emmanuel Mathias maarufu kama MC Pilipili, aliyefariki dunia Novemba 16, 2025 jijini Dodoma, imeeleza kuwa walipofika hospitalini leo asubuhi walijiridhisha mwili wa marehemu ulikuwa na alama za majeraha.

Dada wa marehemu, Veronica Mathias, amesema familia haikupata nafasi ya kuuona mwili mara moja baada ya taarifa za kifo kutokana na majukumu waliyokuwa nayo, lakini walipojiridhisha leo wameona majeraha hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu eneo la Swaswa jijini Dodoma, Veronica amesema familia inasubiri taarifa rasmi kutoka vyombo vya usalama.

Sauti ya Veronica Mathias.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, amesema uchunguzi kuhusu chanzo cha kifo cha MC Pilipili bado unaendelea na taarifa kamili zitatolewa mara baada ya kukamilika.