Dodoma FM
Dodoma FM
14 November 2025, 3:43 pm

Wiki ya Upimaji wa Magonjwa Yasiyoambukiza ilianza Novemba 12 na inahitimishwa leo Novemba 14 katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Na Lilian Leopold.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, amesisitiza umuhimu wa watoa huduma za afya kufuata sheria na sera za serikali ili kuhakikisha wananchi, hususan wazee na mama wajawazito, wanapata huduma stahiki.
Akizungumza katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Upimaji wa Magonjwa Yasiyoambukiza, Shekimweri amesema kufuata taratibu za serikali ni msingi wa kuimarisha huduma za afya na kulinda maisha ya wananchi.

Aidha, amewataka wananchi kuendeleza utamaduni wa kuchangia damu salama, akieleza kuwa kitendo hicho ni msaada muhimu ambao mtu anaweza kuuhitaji wakati wowote anapopatwa na dharura ya kiafya.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania inahitaji takribani chupa 550,000 za damu salama kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa, hususan akina mama wajawazito, watoto wenye upungufu wa damu, na waathirika wa ajali.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma wamelipongeza zoezi hilo la upimaji, wakisema limewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata ushauri muhimu wa kitabibu.
Takwimu za awali zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 85 ya wananchi walioshiriki wamejitokeza kwa hiari kupima na kuchangia damu salama.
Wiki ya Upimaji wa Magonjwa Yasiyoambukiza ilianza Novemba 12 na inahitimishwa leo Novemba 14 katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, ikiwa na kauli mbiu isemayo: “ Chukua hatua, dhibiti magonjwa yasiyoambukiza”