Dodoma FM
Dodoma FM
23 October 2025, 5:07 pm

Sajenti Ester amesema kitendo cha madereva kukatisha ruti bila sababu za msingi ni ukiukwaji wa sheria za usafirishaji wa abiria.
Imeelezwa kuwa kitendo cha baadhi ya madereva wa usafiri wa daladala Jijini Dodoma kukatisha safari zao kabla ya kufika mwisho wa kituo cha mwisho ni kosa kisheria, na mamlaka zimewataka abiria kutoa taarifa pindi wanapobaini vitendo hivyo.
Hayo yamebainishwa na Sajenti Ester Makali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Dawati la Elimu kwa Umma Mkoa wa Dodoma, kufuatia kuwepo kwa vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya madereva na kuwakwaza abiria.
Taswira ya Habari imezungumza na baadhi ya madereva wa daladala jijini Dodoma ili kubaini sababu zinazowafanya baadhi yao kutofika mwisho wa safari zao katika vituo walivyo pangiwa.
Hata hivyo, baadhi ya abiria wameeleza kusikitishwa na tabia hiyo wakisema inawasababishia usumbufu mkubwa ikiwemo kupoteza muda na kuongezeka gharama za usafiri.
Aidha, Sajenti Makali amewataka abiria kutokuwa kimya wanapokutana na madereva wanaokiuka sheria hizo, badala yake watoe taarifa kwa vyombo vya usalama au LATRA ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.
Sajenti Makali amehitimisha kwa kusisitiza kuwa nidhamu barabarani ni msingi wa usalama wa watumiaji wote wa vyombo vya usafiri, na kwamba kila dereva anatakiwa kufuata sheria bila shuruti.