Dodoma FM
Dodoma FM
22 October 2025, 3:50 pm

Hadi sasa, mamlaka mbalimbali zimeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama wa mitandaoni na matumizi sahihi ya teknolojia, huku ikiendelea kuhamasisha matumizi bora ya TEHAMA kwa maendeleo ya jamii.
Na Anwary Shaban.
Wananchi nchini wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya na yenye tija kwa maisha yao, ikiwemo kuitumia kutangaza biashara zao na kujifunza mambo mbalimbali badala ya kusambaza taarifa za uchochezi au kuanzisha vurugu kupitia majukwaa hayo.
Wito huo umetolewa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Wilaya ya Dodoma Mjini, SSP Grace Salia, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika jamii ya sasa.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Jiji la Dodoma, hususan vijana, wameeleza namna wanavyotumia mitandao ya kijamii na intaneti katika shughuli zao za kila siku. Wengi wao wameeleza kuwa mitandao hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kujifunza, kufanya utafiti, na hata kukuza biashara ndogondogo.
Sanjari na hayo, SSP Grace Salia amesisitiza kuwa jeshi la polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa watu watakaotumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa za uongo, chuki au uchochezi, kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kuhatarisha amani ya nchi.