Dodoma FM

Wakulima wa zabibu wapatiwa mafunzo kuongeza ujuzi

21 October 2025, 3:21 pm

Picha ni baadhi ya wakulima wasindikizaji wa zabibu katika mafunzo ya kuongeza ujuzi Picha na Selemani Kodima.

Katika mafunzo hayo yaliyofanyika Hombolo, jijini Dodoma jumla ya wakulima 70 wamepatiwa mafunzo hayo kwa ajili ya kuongeza thamani ya zao la zabibu.

Na Selemani Kodima.

Wakulima na wasindikaji wadogo wa zao la zabibu mkoani Dodoma wamepatiwa mafunzo maalum ya kukuza ujuzi katika mlolongo wa thamani wa zao hilo, yakiwemo masuala ya uvunaji, uhifadhi, uongezaji thamani na mbinu za kutafuta masoko ya zabibu na bidhaa zake.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Hombolo, jijini Dodoma, Afisa Kazi Mkuu Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Neema Moshi, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi na maarifa kwa wakulima na wafanyakazi ili kuendana na mabadiliko ya kisayansi, kiteknolojia na kiuzalishaji.

Awali, akizungumza Mkulima wa Zabibu kutoka Hombolo, Bi. Rachel Mushi, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kujifunza mbinu bora za uhifadhi na usindikaji wa zabibu jambo litakalomwezesha kuongeza kipato kupitia uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa juu.

Naye Bw. Daniel Mgonja, msindikaji mdogo wa zabibu kutoka kijiji cha Nzuguni, amesema kupitia mafunzo hayo amepata uelewa kuhusu ubora wa vifungashio na namna ya kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, inayolenga kuwajengea uwezo wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali, ikianzia na wakulima na wasindikaji wadogo wa zao la Zabibu. Aidha, yanatolewa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).