Dodoma FM
Dodoma FM
17 October 2025, 4:00 pm

Wakati uchaguzi mkuu ukikaribia, vijana wa Chitabuli wametakiwa kujitokeza kupiga kura kwa amani na kuepuka vitendo vya vurugu. Picha na Blogers.
Kwa kufanya hivyo, watakuwa wametimiza haki yao ya msingi, kwani kila kijana ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kwa kupiga kura na kulinda amani ya nchi.
Na Victor Chigwada.
Wakati zikiwa zimesalia siku 12 kuelekea uchaguzi mkuu, vijana wa Kijiji cha Chitabuli, Kata ya Membe, Wilaya ya Chamwino, wametakiwa kujitokeza kushiriki zoezi la uchaguzi kwa amani badala ya kujiingiza kwenye maandamano yanayoweza kuvunja amani.
Wito huo umetolewa na Joseph Chilenga Mwenyekiti wa Kijiji cha Chitabuli, wakati akifanya mahojiano na Taswira ya habari ambapo amesema ni jukumu la kila mtu kupiga kura, hivyo ni muhimu kwa vijana kuhakikisha wanalinda amani kwenye uchaguzi..
Chilenga pia ameonya kuwa matumizi ya dawa ya kulevya ni mojawapo ya sababu zinazoongeza uwezekano wa matendo mabaya miongoni mwa vijana, hivyo ni vyema jamii, hususan kundi la vijana, kujiepusha na matumizi ya madawa hayo.
Baadhi ya vijana hao wamewataka wenzao kuacha kujiingiza katika maandamano yanayoweza kuvunja amani ifikapo Oktoba 29. Pia wameongeza kuwa ni muhimu kushiriki zoezi la uchaguzi kwa amani, kwa kuzingatia mustakabali bora wa Taifa.