Dodoma FM
Dodoma FM
17 October 2025, 3:19 pm

Picha ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum wakati wa uzinduzi wa jengo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) jijini Dodoma. Picha na Anwary Shaban.
Uzinduzi wa TIRA Bima House umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha na bima, wakuu wa taasisi za serikali, pamoja na Tasisi Binafsi.
Na Anwary Shaban.
Imeelezwa kuwa sekta ya bima nchini inaendelea kukua kwa kasi ambapo bima za kawaida zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 79.2 hadi kufikia bilioni 957, hatua inayodhihirisha maendeleo makubwa katika tasnia hiyo muhimu ya uchumi.
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la kisasa la Mamlaka yaUsimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), uliofanyika Oktoba 16 katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma .
Kwa mujibu wa Dkt. Saqware, jengo hilo litakuwa kitovu cha huduma za bima kwa wananchi, ambapo huduma zitakazotolewa ni pamoja na bima za afya, majengo, na huduma nyingine muhimu zinazolenga kuongeza uelewa na ushiriki wa Watanzania katika masuala ya bima.
Dkt. Saqware ameongea kwa kusema asekta ya bima pia imesaidia kuongeza ajira nchini, ambapo ajira rasmi zimeongezeka kwa asilimia 14.9, jambo linaloashiria kuwa sekta hiyo ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, ambaye amesisitiza kuwa bima ni huduma muhimu katika kulinda uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Dkt. Saada pia ameipongeza TIRA kwa kazi kubwa wanayoifanya, usiku na Mchana kuhakikisha sekta ya bima nchini inakuwa imara na inayowafikia wananchi wote.
Kwa mujibu wa TIRA, jengo hilo litawezesha huduma zote muhimu za bima kutolewa kwa ufanisi zaidi, huku likisaidia katika kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya bima kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kati.