Dodoma FM
Dodoma FM
15 October 2025, 3:59 pm

Mafunzo kwa Maafisa Viwanda na Uwekezaji mkoani Dodoma yamelenga kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma kwa wawekezaji kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa ya usajili wa makampuni na biashara.
Na Lilian Leopold.
Maafisa Viwanda na Uwekezaji kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Dodoma wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya mifumo ya usajili wa makampuni na wafanyabiashara, lengo likiwa ni kupunguza urasimu, ucheleweshaji wa huduma, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za uwekezaji.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Kuu za Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa Kanda ya Kati wa TISEZA, Venance Mashiba, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo maafisa biashara kuhusu namna bora ya kutumia mifumo ya kidijitali katika kusajili makampuni na wawekezaji, hatua itakayosaidia kuvutia uwekezaji zaidi katika mkoa wa Dodoma.

Kwa upande wao, baadhi ya maafisa biashara na viwanda kutoka Jiji la Dodoma wamesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa mifumo hiyo, jambo litakalowawezesha kuhamasisha wafanyabiashara wenye vigezo kujisajili ili kunufaika na fursa mbalimbali, ikiwemo punguzo la kodi.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wawekezaji na kukuza uchumi wa mkoa wa Dodoma, huku TISEZA ikiendelea kusimamia jitihada za kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha uwekezaji na maendeleo nchini.