Dodoma FM
Dodoma FM
14 October 2025, 12:36 pm

Hali hiyo imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wakulima na wafanyabiashara hasa msimu wa masika.
Na Victor Chigwada.
Wananchi wa vitongoji vya Mugu na Mjiha, vilivyopo Kata ya Idifu, Wilaya ya Chamwino, wameiomba serikali kujenga daraja katika eneo la Nyika, ambalo limekuwa changamoto kubwa nyakati za mvua kutokana na kujaa maji.
Wamesema kuwa eneo hilo linatenganisha kijiji katika pande mbili, ambapo upande mmoja una makazi ya watu wengi, huku upande mwingine ukiwa na mashamba makubwa ya kilimo. Hali hiyo imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wakulima na wafanyabiashara hasa msimu wa masika.
Wananchi hao wameeleza kuwa maji yanapokuwa yamejaa, shughuli za kiuchumi hufikia kusimama kabisa, huku baadhi ya mashamba kupata hasara kubwa kutokana na kutofikika. Wanafunzi pia wameripotiwa kushindwa kuvuka kwenda shule, jambo linaloathiri elimu yao.
Wameongeza kuwa kila inapofika msimu wa mvua, wakazi hulazimika kukaa nyumbani kwa kukosa usafiri wa kuvuka eneo hilo, hali inayosababisha usumbufu mkubwa katika maisha yao ya kila siku.
Kwa mujibu wa wananchi hao, changamoto hiyo imekuwa ya muda mrefu, hivyo wameitaka Serikali kuanza kuchukua hatua za haraka za ujenzi wa daraja litakalorahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.