Dodoma FM
Dodoma FM
13 October 2025, 10:06 am

Hatua hii itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuimarisha mazingira ya kujifunzia. Picha na Mtandao.
Kupitia mradi wa BOOST, serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kujenga na kukarabati vyumba vya madarasa nchi nzima.
Na Victor Chigwada.
Wananchi wa Kijiji cha Mjeloo, Kata ya Handali, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wameishukuru serikali kwa ujenzi wa vyumba 16 vya madarasa katika shule ya msingi, hatua iliyosaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuimarisha mazingira ya kujifunzia.
Wakizungumza na Dodoma FM, wananchi hao wamesema ujenzi wa vyumba hivyo umepunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule mama, na kuongeza hamasa ya watoto kujifunza.
Wameeleza kuwa madarasa hayo mapya yataboresha kiwango cha elimu kwa wanafunzi kutokana na kuwawezesha kusoma katika mazingira rafiki na yenye utulivu.
Aidha, wamewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha wanatumia vyema fursa zinazotolewa na serikali kwa kuhakikisha watoto wote wanahudhuria shule, wakisisitiza kuwa watoto wanaoachwa mitaani huishia kujiingiza katika makundi yasiyo na maadili, jambo linaloweza kuathiri mustakabali wa jamii.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mjeloo, Ndg. Emmanuel Tanaga, ameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu, akisema ujenzi huo ni uwekezaji mkubwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kutekeleza mradi wa BOOST, unaolenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora kuanzia ngazi ya awali hadi shule za msingi, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa vya kujifunzia.