Dodoma FM
Dodoma FM
9 October 2025, 10:31 am

Picha ni baadhi wa wananchi wakiwa na mifugo yao katika Mnada wa Mbalawala. Picha na Lilian Leopold.
Katika ziara hiyo, timu ya watumishi wa kanda ilishiriki katika shughuli za makusanyo ya ushuru wa mifugo, biashara ndogo ndogo, pamoja na utoaji wa elimu ya usafi na utunzaji wa mazingira kwa wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo.
Na Lilian Leopold.
Kanda Namba Tatu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanya ziara katika mnada wa Mbalawala kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kanda hiyo.
Katika ziara hiyo, timu ya watumishi wa kanda ilishiriki katika shughuli za makusanyo ya ushuru wa mifugo, biashara ndogo ndogo, pamoja na utoaji wa elimu ya usafi na utunzaji wa mazingira kwa wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Manunuzi wa kanda namba tatu, Shakila Mwanyembe, amesema lengo la mnada huo ni kufanya ukaguzi, kuratibu na kusimamia mapato ya jiji, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa ushuru na kupata vibali halali vya mifugo.

Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa kanda namba tatu, Ivan Kamuna, amesema wananchi wameonyesha mwamko mzuri katika elimu waliyopewa na wameomba elimu kama hiyo iendelee kutolewa mara kwa mara ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao ipasavyo katika ulipaji wa kodi.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Muungano, Athanasio Madole, ameishukuru halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, ikiwemo utoaji wa leseni na vibali, hatua iliyopunguza adha ya kusafiri hadi ofisi kuu za jiji kufuata huduma hizo.
Ziara hiyo imekuwa fursa kwa kanda namba tatu kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kukuza uwajibikaji kwa wananchi katika ulipaji wa ushuru. Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuboresha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi.