Dodoma FM

Watoto hatarini kwa imani potofu za meno ya plastiki

8 October 2025, 10:23 am

Vitendo hivyo vimeripotiwa kusababisha maumivu makali, upotevu mkubwa wa damu, na wakati mwingine vifo kwa watoto wadogo. Picha na Google.

Aidha, ripoti ya kimataifa ya mwaka 2023 kuhusu afya ya kinywa barani Afrika inaonyesha kuwa zaidi ya watoto 1 kati ya 10 katika baadhi ya maeneo ya Tanzania hupoteza maisha au hupata maambukizi makubwa kutokana na vitendo hivyo vinavyofanywa bila utaalamu.

Na Peter Nnunduma.

Baadhi ya jamii bado zinaamini kuwa watoto huzaliwa na meno ya plastiki, jambo linalosababisha wazazi na walezi kuchukua hatua hatarishi za kuyakata meno hayo kwa kutumia njia za kimila na vifaa visivyo salama.

Vitendo hivyo vimeripotiwa kusababisha maumivu makali, upotevu mkubwa wa damu, na wakati mwingine vifo kwa watoto wadogo.

Akizungumza na Taswira ya Habari, Daktari wa Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Justine Eliudi, amesema huduma za afya ya kinywa zinapatikana na ni salama, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi kutafuta ushauri wa kitaalamu badala ya kutumia njia za kimila ambazo huweka maisha ya watoto hatarini.

Sauti ya Dkt. Justine Eliudi.

Ameongeza kuwa wataalamu wa afya wameendelea kutoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto hospitalini mara wanapobaini mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida katika kinywa au fizi badala ya kutumia imani za kimila ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya watoto.

Utafiti uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na taasisi ya Bridge2Aid mwaka 2022, umebaini kuwa takribani asilimia 9 hadi 17 ya watoto nchini wamewahi kufanyiwa vitendo vya kukata meno ya plastiki kwa njia za kienyeji.