Dodoma FM
Dodoma FM
2 October 2025, 1:23 pm

Kupitia mfumo wa NeST, vikundi vya kijamii sasa vinaweza kushiriki kikamilifu katika manunuzi ya serikali kupitia usajili mtandaoni, kuomba zabuni, na kufuatilia hatua za maombi yao.
Na Lilian Leopold .
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanya kikao na vikundi mbalimbali vya kijamii kwa lengo la kuwaelimisha jinsi ya kujisajili na kutumia mfumo wa manunuzi ya serikali, maarufu kama NeST.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Oktoba 01 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Dodoma, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ally Mfinanga, amesema kupitia mfumo huo vikundi vitapata nafasi ya kujisajili na kuomba kazi zinazotolewa na serikali.

Miongoni mwa washiriki waliohudhuria mafunzo hayo walikuwa Warda Kisaka, mwanachama wa kikundi cha Wabunifu, na John Samwel, Mwenyekiti wa kikundi cha Mwamko Vijana Kiuchumi, ambao wamesema mfumo huo utawarahisishia kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali.
Aidha, washiriki hao wamewataka wananchi wote kuchangamkia fursa za mafunzo hayo, kwani ni nafasi muhimu kwa vikundi na wananchi kujifunza namna ya kushiriki kikamilifu katika manunuzi ya serikali.
Kupitia mfumo wa NeST, vikundi vya kijamii sasa vinaweza kushiriki kikamilifu katika manunuzi ya serikali kupitia usajili mtandaoni, kuomba zabuni, na kufuatilia hatua za maombi yao. Mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa taarifa, unakuza uwazi na uwajibikaji, na pia unatoa fursa sawa kwa vikundi vidogo, vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za kiuchumi zinazotolewa na serikali.