Dodoma FM

Serikali, wadau waja na mikakati kilimo biashara

30 September 2025, 2:34 pm

Mradi wa VKB unatarajia kunufaisha zaidi ya vijana 40,000 kutoka mikoa ya Singida na Dodoma.Picha na Seleman Kodima.

Kupitia mradi huo, vijana wanapewa mafunzo ya kilimo chenye tija, ujasiriamali, elimu ya fedha, na uelewa wa mnyororo wa thamani wa mazao.

Na Seleman Kodima.

Licha ya sekta ya kilimo kuchangia ajira kwa Watanzania kwa Asilimia 65.5, bado imeendelea kukumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi ya zana duni, teknolojia hafifu, kukosekana kwa masoko ya uhakika, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hali hiyo imekuwa kikwazo kwa wakulima wengi, hususan vijana, kushiriki kikamilifu katika kilimo chenye tija.

Hata hivyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kufungua fursa za kilimo biashara kwa vijana, kama njia ya kupunguza tatizo la ajira na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Sekta ya kilimo imebainika kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa, ambapo inatoa asilimia 65.5 ya ajira nchini na kuchangia asilimia 65 ya malighafi kwa sekta ya viwanda.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 pamoja na Utafiti wa Hali ya Nguvu Kazi wa mwaka 2021, Tanzania ina takriban vijana milioni 14.2 wenye uwezo wa kufanya kazi, sawa na asilimia 55 ya nguvu kazi yote ya Taifa. Kati ya hao, asilimia 31 wanatoka kwenye kundi la vijana, jambo linaloonesha umuhimu wa kuwashawishi kushiriki kikamilifu katika kilimo biashara.

Akizungumza kuhusu nafasi ya vijana katika kilimo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen Nindi, amesema sensa imeonesha kundi la vijana lina nguvu kazi kubwa ambayo ikielekezwa vizuri inaweza kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.

Sauti ya Dkt. Stephen Nindi.

Moja ya miradi inayotekelezwa ni Mradi wa Vijana Kilimo Biashara (VKB) unaosimamiwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na Shirika la Rikolto.

Afisa Miradi wa VKB kutoka WFP, Bi Mboka Mwanitu, amesema hadi sasa wamefanikiwa kuwafikia vijana 83,000, ambapo asilimia 70 ni wanawake. Mazao yanayoangaziwa ni mtama, alizeti, mbogamboga na matunda.

Sauti ya Bi Mboka Mwanitu.

Afisa kutoka Shirika la Rikolto Willifaston Ntoroma  ameongeza kuwa asilimia kubwa ya wanufaika wa mradi ni wanawake, ikiwa ni mkakati wa kuondoa mitazamo hasi ya kijamii kuhusu ushiriki wa wanawake katika kilimo biashara. Hadi sasa, vijana 27 kati ya 100 kutoka mikoa ya Singida na Dodoma wameonesha mawazo ya kibiashara yanayoweza kuongeza uzalishaji.

Sauti ya Willifaston Ntoroma .

Baadhi ya vijana walionufaika na mradi huo, akiwemo Geofrey Sanga na Lucy Kitwange, wamesema changamoto kama zana duni, mitaji midogo, na mitazamo hasi kuhusu kilimo bado zinawakwamisha vijana wengi kuingia kwenye sekta hiyo.

Sauti za Geofrey Sanga na Lucy Kitwange.

Ikumbukwe kuwa Mradi wa VKB unatarajia kunufaisha zaidi ya vijana 40,000 kutoka mikoa ya Singida na Dodoma, wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35, ambapo asilimia 70 ya wanufaika ni wanawake.