Dodoma FM
Dodoma FM
30 September 2025, 1:16 pm

Jitihada hizo pia zimeongeza ufanisi wa ufundishaji, ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kufundishia vilivyoboreshwa kupitia michango ya wazazi.
Na Victor Chigwada.
Imeelezwa kuwa jitihada za wazazi katika Shule ya Sekondari Ihumwa zimekuwa chachu ya kuongeza upatikanaji wa walimu wa masomo ya sayansi shuleni hapo.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Bi. Tumain Kivuyu, amesema hatua hiyo imechochea maendeleo makubwa katika kufanikisha mahitaji ya walimu, hasa kwa kuzingatia kuwa changamoto ya walimu wa sayansi ilikuwa tishio kubwa.
Amesema wazazi walilazimika kuchanga fedha kwa ajili ya kuwalipa walimu wa ziada, hatua iliyosaidia kupunguza tatizo hilo. Aidha, ameongeza kuwa jamii inahitaji kila aina ya wataalamu, hivyo kukosekana kwa walimu wa sayansi kungeweza kuathiri vibaya mustakabali wa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Batholomeo Gasper, amesema kuwa mchango wa wazazi umesaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi, ukilinganisha matokeo ya mwaka 2023/24 na 2024/25.