Dodoma FM
Dodoma FM
10 September 2025, 3:10 pm

TANESCO imewataka wananchi wote waliounganishiwa umeme kwa njia zisizo halali kujitokeza mara moja kwa hiari ili kusafisha taarifa zao, huku ikisisitiza kuwa operesheni hiyo itaendeleakatika mikoa mingine ili kudhibiti wizi wa umeme nchini.
Na Anwary Shaban.
Mkazi mmoja wa Jiji la Dodoma amejikuta matatani baada ya kubainika kuwa alikuwa akitumia umeme kwa njia isiyo halali kwa zaidi ya miaka miwili kupitia mita ya wizi maarufu kama “kishoka”.
Tukio hilo limebainika katika msako maalum uliofanywa na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), ukilenga kuwabaini wakazi waliounganishiwa umeme kinyume cha taratibu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Akizungumza mkazi huyo alikiri kutumia mita hiyo haramu kwa muda mrefu, akieleza kuwa alikosa uelewa wa taratibu sahihi za kuunganishiwa umeme kutoka TANESCO, huku akidai kuwa alikumbwa na changamoto ya kupata huduma hiyo kwa haraka.
Kwa mujibu wa maofisa wa TANESCO, matumizi ya mita za kishoka yamesababisha hasara kubwa kwa shirika hilo na kuhatarisha maisha ya wananchi, kutokana na miunganisho isiyo salama ya umeme.