Dodoma FM
Dodoma FM
16 July 2025, 1:54 pm

Lugha za matusi na udhalilishaji majukwaani zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake wanaotaka kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi. Hali hii inaathiri si tu ushiriki wao, bali pia inadhoofisha demokrasia jumuishi na haki za binadamu.
Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, Haki za Wanawake Katika Tathmini, Miaka 30 Baada ya Beijing, inaonesha kuwa licha ya maendeleo makubwa, kufikia mwaka 2024 karibu robo ya serikali duniani ziliripoti kurudi nyuma kwa haki za wanawake.
Ripoti hii iliyotangazwa kabla ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi, inasisitiza jinsi haki za wanawake na wasichana zinakabiliwa na hali isiyo ya kawaida ya vitisho vinavyozidi kuongezeka. Kuanzia viwango vya juu vya ubaguzi hadi ulinzi dhaifu wa kisheria, na ufadhili mdogo kwa programu na taasisi zinazounga mkono na kulinda wanawake.

Taasisi ya Kitaifa ya Kidemokrasia (NDI), katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wanawake waliochaguliwa kwa nafasi za ubunge ni asilimia 9.5, wabunge wa viti maalumu ni asilimia 29, hivyo kufanya jumla ya wabunge wanawake kuwa 142 kati ya 393.
Vilevile, ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya mwaka 2020 inaonesha wanawake waliochaguliwa kwa nafasi za udiwani walikuwa asilimia 6.58 (260 kati ya madiwani 3,953), viti maalum walikuwa 1,374 katika halmashauri 184 sawa na asilimia 24.59. Kwa jumla, wanawake walikuwa asilimia 29.24 ya madiwani wote nchi nzima.
Ripoti ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2019 pia inaonesha kuwa kati ya nafasi 11,915 za wenyeviti wa vijiji, wanawake walishinda nafasi 246 sawa na asilimia 2.1, huku wanaume wakishika asilimia 97.9 ya nafasi hizo. Kati ya nafasi 4,171 za wenyeviti wa mitaa, wanawake walishinda nafasi 528 sawa na asilimia 12.6.