Dodoma FM
Dodoma FM
23 April 2025, 1:31 pm

Tadio huendesha mafunzo mara kwa mara kwa waandishi wa habari kutoka redio wanachama ili kuwajengea uwezo hasa utangazaji wa kidijitali.
Na Saumu Bakari
Taasisi ya Maendeleo ya Vyombo vya Habari vya Kijamii TADIO imeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka redio wanachama wapya namna ya kuchapisha habari mtandaoni. Mafunzo hayo yanafanyikia jijini Dodoma.
Akifungua mafunzo hayo, Meneja Miradi wa Tadio Bi. Saumu Bakari amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kutumia jukwaa la habari mtandaoni radiotadio.co.tz kufikia wasomaji wengi zaidi popote walipo duniani. Ameongeza kuwa Tadio itaendelea kuwa mlezi wa redio jamii na kuzipatia mafunzo ya mara kwa mara.

Kwa upande wake Mhariri Mkuu wa jukwaa hilo Bw. Hilali Ruhundwa amesema kuwa Tadio imeunganisha redio jamii nyingi nchini na kuzifanya zishirikishane habari za maeneo waliyopo. Aidha amewataka kutumia jukwaa hilo kikamilifu kwa manufa ya jamii wanayoihudumia.
Naye Afisa Tehama Bw. Amua Rushita amesema mafunzo hayo yatafanyika kila mara ikiwemo kuwatembelea kwenye vituo vyao vya redio kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kutumia mtandao.
Washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza Tadio na wameahidi kutumia jukwaa hilo kupashana habari za vijijini.
Mafunzo hayo ya siku mbili ni mwendelezo wa mafunzo ya mara kwa mara ambayo huendeshwa na Tadio kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Vyombo vya Habari wa nchini Finland ambapo waandishi wa habari kutoka redio wananchama ili kuendana na teknolojia ya sasa.