

12 February 2025, 4:53 pm
Ikumbukwe kuwa Ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi, teknolojia, uhandisi, hisabati bado ni mdogo licha ya juhudi za wadau katika eneo hilo.
Na Seleman Kodima.
Dhana Potofu imetajwa kuendelea kuwa kikwazo kinachokwamisha juhudi za wanawake na wasichana kusoma masomo ya sayansi.
Kwa mujibu wa Takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 24 pekee ya wanafunzi wa kike walioko vyuoni wanasoma masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
Katika kufahamu nini kifanyike ili kuongeza hamasa ya wanawake na wasichana kusoma masomo ya Sayansi ,Taswira ya Habari tumefanya Mahojiano na mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Dodoma UDOM Dkt Rehema Ulimboka na hapa amezungumza na mwandishi wetu Selemani kodima kwa njia ya simu.
Mapema jana katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira, na Watu Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema ongezeko la wanawake na wasichana katika nyanja za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati (STEM) litasaidia taifa kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii.
Amesema ni muhimu kuweka mikakati ya kuhamasisha wanawake kushiriki katika masomo ya sayansi, kwani ushiriki wao ni hitaji la muda mrefu kwa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta za sayansi, uhandisi, na hisabati, ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii.