Ujenzi wa miundombinu Kiteto kufungua uchumi wa wilaya hiyo
7 January 2025, 4:15 pm
Elimu ya mara kwa mara kwa wananchi wa Kiteto ili kuitunza miundombinu hiyo ambayo Serikali imetoa fedha nyingi kuijenga ili iweze kudumu kwa manufaa yao.
Na Selelman Kodima.
Wananchi Wilayani Kiteto mkoani Manyara wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja ambao utasaidia kufungua uchumi wa wilaya hiyo.
Wakizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo wananchi hao wamesema awali kabla ya ujenzi wa miundombinu hiyo walikuwa wakikumbana na changamoto za usafiri na usafirishaji bidhaa hasa mazao.
Akizungumzia kuhusu miradi ya Barabara na madaraja wilayani humo Meneja wa Tarura Wilaya ya KIteto, Mhandisi Edwin Magiri amesema Tarura inahudumia mtandao wa Barabara wenye jumla ya Kilometa 1,291.137, kati ya hizo Kilometa 200.3 ni changarawe, Kilometa 5.128 barabara za lami na Kilometa zaidi ya 1,014 ni barabara za vumbi.
Aidha, amesema licha ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu hiyo, lakini pia wanatoa rai na elimu ya mara kwa mara kwa wananchi wa Kiteto kuhusu kuitunza miundombinu hiyo ambayo Serikali imetoa fedha nyingi kuijenga ili iweze kudumu kwa manufaa yao.