Imani za kishirikina zatajwa kuchangia ukatili dhidi ya Watoto
4 December 2024, 12:29 pm
Kwa Mujibu wa Ofisi ya Maendeleo ya Jamii mwaka 2024 pekee, kwa kipindi cha kuanzaia mwezi wa kwanza hadi mwezi wa nane matukio ya ukatili yaliyoripotiwa mkoa wa Dodoma ni 2,352, ambapo ukatili kwa watoto ni 629 huku watu wazima ni matukio 1,723, wanaume 350 na wanawake 1,373.
Na Ramadhan Idd
Tamaa za kimwili na Imani za kishirikina zimetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu za kukithiri vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto ya Mkoani wa Dodoma.
Hayo yamebainishwa na Elvira Mutagwaba ambaye ni Afisa ustawi jamii Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kitengo cha Huduma Jumuishi Maarufu kama ONE STOP CENTRE, wakati anazungumza na Taswira ya Habari.
Mutagwaba amebainisha kuwa maeneo yaliyoathirika na ukatili wa Kingono ni Dodoma Mjini na wahanga wakubwa ni watoto.
Ukatili huo ambao huathiri afya ya mwili na saikolojia ya manusura, unatajwa kukithiri zaidi kuanzia ngazi ya familia, hali ambayo Jeshi la Polisi hupata wakati mgumu wa kukamata na kuwachukulia hatua watuhumiwa wa vitendo hivyo.
Sambamba na Jitihada zinafanywa na serikali, hivi karibuni baadhi ya wananchi Jijini Dodoma wameomba elimu iendelee kutolewa ili kuepukana na mazoea ya kukumbatia watuhumiwa wa vitendo vya ukatili.