FAWE yaja na mkakati wa masomo ya sayansi kwa watoto
2 December 2024, 11:22 am
Mpango huo, wenye kauli mbiu “Kuwezesha Kila Mwanafunzi Kuziba Mapengo ili Kujenga Siku Zijazo,” unahimiza ushirikiano wa jamii, Serikali na wadau mbalimbali wa elimu.
Na Mariam Kasawa.
Shirika la Wanawake Waelimishaji Afrika (Fawe) limezindua mpango mkakati wa miaka mitano (2024-2028), unaolenga kuwawezesha watoto wa kike na wa kiume kusoma masomo ya sayansi, ili kuziba pengo la kitaaluma na kuzalisha wataalamu zaidi nchini.
Mratibu wa Taifa wa Fawe Tanzania, Neema Kitundu, akizungumza wakati wa uzinduzi huo Novemba 29, 2024 jijini Dar es Salaam amesema mpango huo umebuniwa ili kupambana na changamoto za mila na desturi zinazokwamisha elimu kwa watoto wa kike na wa kiume.
Profesa Verdiana Masanja, mmoja wa waanzilishi wa Fawe, amesitiza umuhimu wa elimu kwa mabinti, akisema: “Mkakati huu utahakikisha wasichana na wavulana hawaachwi nyuma kwenye elimu.’’