Wanafunzi walalamika kukataliwa katika baadhi ya vyombo vya usafiri
19 July 2024, 6:27 pm
Licha ya kupanda na kushuka kwa bei ya nishati ya mafuta ya petroli Nchini kunakochangia ongezeko la bei za nauli katika vyombo vya usafiri ikiwemo daladala lakini mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa ardhini LATRA haijabadili kiwango cha nauli kwa wanafunzi cha shilingi 200.
Na Mwandishi wetu.
Baadhi ya wanafunzi katika Jiji la Dodoma wamelalamikia usumbufu wanaoupata kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wakiwemo madereva wa daladala pindi wanapohitaji kupanda vyombo hivyo kuwahi shuleni nyakati za asubuhi na jioni watokapo masomoni.
Baadhi ya wanafunzi hao akiwemo alfa agrey pamoja na jailos ruben wamezungumza na Dodoma TV na kueleza kuwa changamoto ya kukataliwa katika baadhi ya vyombo vya usafiri imekuwepo kwa muda.
Wamesema hatua hiyo inawarudisha nyuma kitaaluma kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta usafiri na wakati mwingine kuchelewa masomo darasani.
Khamis ally ni moja ya dereva wa daladala katika jiji la Dodoma amezungumza na kituo hiki juu ya tuhuma hizo na kueleza kuwa utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi ni chanzo cha kubaguliwa katika vyombo hivyo.
Sarah William mkazi wa kata ya mkonze Jijini Dodoma kama mzazi anasema hatua ya kukataliwa kwa waanfunzi katika vyombo vya usafiri inachangia hofu kwa wazazi juu ya usalama wa watoto wao.