Wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda waomba eneo la soko
22 February 2023, 4:40 pm
Wafanyabiashara wa matunda na mbogamboga wilayani Bahi mkoani Dodoma wameiomba serikali wilayani humo kuwatengea eneo rasmi la kufanyia biashara.
Na Bernad Magawa.
Wafanyabiashara wa matunda na mbogamboga wilayani Bahi mkoani Dodoma wameiomba serikali wilayani humo kuwatengea eneo rasmi la kufanyia biashara ili waweze kuondokana na adha ya kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi ambayo wamesema mengine yanahatarisha maisha yao.
Wafanyabiashara hao wameyasema hayo februali 22,2023 wilayani Bahi wakati wakizungumza na kituo hiki na kueleza kuwa hawana maeneo rasmi ya kufanyia biashara za mbogamboga na matunda na badala yake wamekuwa wakifanyia biashara katika maeneo ya nyumba za watu binafsi, nje ya maduka na mashine za kusaga nafaka kwa makubaliano na wamiliki wa maeneo hayo.
Wamesema pamoja na kufanyia biashara kwenye maeneo ya watu binafsi maeneo hayo mengine yapo pembezoni mwa barabara na kueleza kuwa ni hatari endapo itatokea ajali ya gari maisha yao yanakuwa hatarini na kuiomba serikali kutenga eneo la soko ambalo litawakusanya wafanyabiashara wote kuwa pamoja na kuondokana na adha ya kujihifadhi kwa watu binafsi.
“Tunauomba uongozi wetu wa wilaya ya Bahi ututengee eneo la kufanyia biashara ambalo halipo mbali na mkusanyiko wa watu”
“Tunauomba uongozi wetu wa wilaya ya Bahi ututengee eneo la kufanyia biashara ambalo halipo mbali na mkusanyiko wa watu, tupate eneo zuri kwa biashara zetu kwani kwa sasa tunahangaika kuomba hifadhi za kibiashara kwenye vieneo vya watu binafsi, ikitokea umekosana na aliyekupa hifadhi anakufukuza hivyo mazingira ya biashara zetu ni magumu sana.”
Wakizungumzia zaidi kuhusiana na mazingira ya kufanyia biashara kwa sharti la kutotajwa majina wakihofia kufukuzwa katika maeneo hayo, wamesema wafanyabiashara wengi wa matunda na mbogamboga hawana maeneo ya biashara zao hali inayowalazimu kutembeza biashara zao nyumba kwa nyumba hivyo wameiomba serikali wilayani Bahi kuwasaidia eneo la biashara ili watue mabeseni yao eneo moja.
“Wafanyabiashara tupo wengi sana lakini wengine wanafanyia biashara zao pembezoni mwa barabara, wengine kule kona na wengine kule nyuma kabisa ya eneo hili kwenye eneo la mtu, sisi tunajibanza popote tunapopata kaeneo lakini ni maeneo ya watu binafsi, tunaiomba sana serikali ituhurumie tupate eneo ili tukusanyike pamoja kwani wenzetu wengine wanazunguka na mabeseni mitaani sababu wamekosa maeneo ya kujishikiza”.
Wamesema likipatikana soko litawarahisishia wao kuagiza bidhaa za kutosha tofauti na sasa ambapo wanalazimika kuagiza kiasi kidogo sana cha bidhaa kwa hofu ya usalama wa maeneo wanayofanyia biashara ambayo yana usalama mdogo kwa mizigo yao hali inayowarudisha nyuma kiuchumi.