Jamii imetakiwa kuzingatia umuhimu wa afya kwa kupima mara kwa mara
1 November 2021, 11:21 am
Na;Shani Nicolous.
Wito umetolewa kwa jamii kuzingatia masuala ya kiafya katika umuhimu wake kwa kupima afya zao mara kwa mara.
Wito huo umetolewa na Mwasisi na Rais kutoka shirika la afya ya akili CMHI Dr. Joshua John amesema kuwa kuna umuhimu wa kufuatilia afya mapema hususani afya ya uzazi kwa mama na mtoto ili kujikinga na baadhi ya maradhi kabla ya matokeo mabaya.
Amesema kuwa watoto chini ya miaka mitano wapo hatarini kupata maradhi mbalimbali lakini ni rahisi kupona endapo mtoto anakinga anazopewa kliniki, endapo mzazi hakufuatilia afya ya mtoto wake mapema ni rahisi kupoteza uhai wa mtoto.
Ameongeza kuwa wanawake wengi wanachukulia kawaida kutokuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mama mjamzito na husababisha vifo kwa mama ma mtoto.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi jijini hapa wamesema kuwa kuna umuhimu serikali na mamlaka za afya kutoa elimu mfululizo katika jamii juu ya afya ya mama na mtoto hususani vijijini ili kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima.
Kwa mujibu wa takwimu za mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia Watoto duniani UNICEF na Shirika la Afya Duniani WHO 2017 -2018 ,Wanawake na watoto wachanga ndio wako kwenye hatari wakati na mara tu baada ya kuzaliwa.