Wananchi watakiwa kushirikishwa kuweka mifumo bora ya kisera na kisheria
23 October 2021, 2:48 pm
Na;Yussuph Hans.
Asasi za kiraia Nchini zimetakiwa kuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa kuisadia Serikali katika mipango mbalimbali ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Rasilimali Racheal Chagonja wakati akizungumza na Dodoma Fm katika Maonesho ya Wiki ya Asasi za kirai yanayofanyika Mkoani Dodoma.
Bi Chagonja amesema kuwa kuna utajiri mkubwa katika Rasimali, hivyo ni vyema Watanzania wakashirikishwa pamoja na Serikali kuweka Mifumo bora ya kisera na kisheria.
Naye Atupele Fredy Mwakibete Mbunge wa Jimbo la Busekelo na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa Mitaji ya Umma, amepongeza Haki Rasilimali namna ambavyo wanatoa elimu kwa Jamii ikiwa ni pamoja na kusaidia Wanawake zaidi ya 2000 Wachimbaji Madini na kuwatafutia Masoko.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania TAWOMA Salma Ernest amesema kulingana na elimu ambayo wameipata imewasaidia kwa kiasi kikubwa huku akishukuru Serikali kwa jitihada zinazoendelea kufanyika.
Maonesho ya Wiki ya Asasi za kiraia yamefunguliwa leo Jijini Dodoma na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Joab Ndugai yalioenda sambamba na kauli mbiu Isemayo “Azaki Na Maendeleo”