Msamalo wamshukuru waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani
20 August 2021, 12:42 pm
Na; Selemani Kodima .
Uongozi wa kata ya Msamalo wilayani Chamwino umetoa shukrani kwa Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani kwa jitahada kubwa ambazo zimeendelea kufanywa kuhakikisha vijijiji vinavyopatikana katika kata hiyo vinapata huduma ya Umeme.
Hayo yamesemwa na Diwani wa kata ya Msamalo Bw. Elias Kawea amesema kupitia Ziara ya Waziri wa nishati ambayo aliifanya mwaka Jana katika Kata yake imekuwa na mafanikio makubwa katika upatikanaji wa umeme kwa wakazi wa msamalo.
Amesema katika Vijiji vya Mnase, Mgunga, Mlebe, na Msamalo wameendelea kushuhudia mradi wa usambazaji umeme Vijijini ukiendelea huku baadhi ya Vitongoji vichache ikiwemo Mgondo, Mvunda na Majengo mapya vikiwa bado havijapelekewa Umeme.
Aidha amesema mafanikio ya upatikanaji wa umeme katika Kata yake ni ushirikishwaji wa watalaamu wa Umeme pamoja shirika la Umeme Tanzania Tanesco katika Masuala yote yanayohusu huduma hiyo.
Pamoja na hayo amewahakikishia wananchi wa maeneo hayo ambayo bado hawajapata huduma ya umeme kuwa zoezi la usambazaji wa umeme bado linaendelea hivyo kila mmoja atapata huduma hiyo.