Wakazi wa Chitabuli watakiwa kujiandaa kupokea mradi wa ujenzi wa daraja na barabara
19 August 2021, 12:52 pm
Na; Selemani Kodima.
Wakazi wa kijiji cha Chitabuli Kata ya Membe Wilayani Chamwino wametakiwa kujiandaa kupokea mradi wa ujenzi wa daraja pamoja na barabara inayounganisha Kijiji hicho na Kijiji cha Membe.
Akizungumza na Taswira ya Habari Diwani wa Kata ya Membe Saimon Macheo amesema kuwa tayari bajeti ya ujenzi wa daraja hilo imetolewa hivyo ni muda wa kusubiri utakelezaji wa wakandarasi kuanza kufanya kazi ya ujenzi.
Bw. Macheo amesema ni mapema kubainisha bajeti iliyopitishwa kutokana na hali halisi ya tathimini ambayo inategemea kufanyika kwa kuzingatia ujenzi wa daraja pamoja na ukarabati wa sehemu korofi katika barabara ya membe- chitabuli.
Aidha amesema walitegemea kutembelewa na Mbunge wa Jimbo la chamwino kwa ajili ya kuzungumza na wakazi wa Chitabuli na kuweka bayana mikakati ya utatuzi wa changamoto hiyo
Pamoja na hayo amewataka wakazi wa Chitabuli kutoa ushirikiano pale ambapo wakandarasi watakapoanza ujenzi wa daraja hilo.
Ikumbukwe kuwa Kijiji cha Chitabuli ni moja ya Vijiji ambavyo vinapitia wakati mgumu hususani katika msimu wa mvua kutokana na uwepo wa korongo kubwa ambalo hujaa maji na kusababisha wakazi wa eneo hilo kuishi kama wapo Kisiwani.