Jamii imetakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona
8 July 2021, 1:15 pm
Na; Benard Filbert.
Jamii imetakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kwa mujibu wa maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na Serikali pamoja na wataalamu wa afya.
Wito huo umetolewa na afisa afya wa Jiji la Dodoma Bw. Abdallah Mahiya wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu muongozo wa Jiji katika kupambana na ugonjwa huo.
Amesema Jiji la Dodoma linaendelea na kampeni ya kuhakikisha ugonjwa huo hauathiri wakazi wa Mkoa wa Dodoma ambapo wamejikita katika kutoa elimu zaidi kwa kila mmoja ili kuwa na uelewa.
Amesisitiza watu wanaoenda katika vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanavaa barakoa kwani ni utaratibu uliopangwa Nchi nzima kufanya hivyo huku akikumbusha umuhimu wa kufanya mazoezi ili kuimarisha kinga za mwili.
Baadhi ya wananchi ndani ya jiji la Dodoma wamesema ni vyema kuchukua tahadhari ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kwani ni hatari.
Mapema hapo jana Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluh Hassan akizungumza na wakazi wa Kibaigwa akiwa njiani kuelekea Mkoani Morogoro alinukuliwa akisema ni vyema watu wakazingatia kuvaa barakoa hususani kwenye meneo ya mikusanyiko ili kujikinga na maambuizi hayo.