Tanzania yazindua mpango wa Tatu wa maendeleo ya Taifa
29 June 2021, 12:56 pm
Na;Yussuph Hans.
Tanzania imezindua mpango wa tatu wa Maendeleo kwa Taifa wa miaka mitano 2021 – 2026.
Mpango wa tatu wa maendeleo ya Taifa umegharimu Tsh Trilion 114.8, sekta binafsi ikichangia Tsh Trilion 40.6 huku sekta ya umma ikichangia Tsh Trilioni 74.2.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa akiwa katika uzinduzi huo amezungumzia mafanikio yaliyopatikana kupitia Mpango wa Pili wa Taifa ambao ulipelekea Tanzania kuingia katika uchumi wa kati.
Aidha amebainisha changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na upungufu wa ajira za uhakika, mabadiliko ya tabia nchi na mdororo wa uchumi.
Muwakilishi wa Sekta binafsi Isaac Mbena amesema wapo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali hasa kutokana na vipaumbele vya Mpango wa tatu kuwagusa zaidi.
Awali akifungua mkutano Katibu Mkuu wa Hazina Bw. Emmanuel Tutuba amesema mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa umejikita katika maeneo Makuu Matano ambayo ni makusudio ya Serikali katika kuleta maendeleo ndani ya Nchi.
Uzinduzi wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa umeenda sambamba na kauli mbiu inayosema “kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu”