Malalamiko ya uchaguzi wa tahasusi kwa wanafunzi wa kidato cha tano ni upotoshaji
8 June 2021, 10:35 am
Na; Mariam Matundu.
Imeelezwa kuwa malalamiko mengi yanayotolewa na wananchi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uchaguzi wa tahasusi kwa wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu ni ya upotoshaji .
Hayo yameelezwa hii leo na waratibu wasaidizi wa zoezi la uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha tano wakati wakitolea ufafanuzi juu ya malalamiko ya baadhi ya wanafunzi na wazazi yanayoendelea katika mitandao ya kijamii.
Maxmillan Modest ni afisa elimu idara ya elimu Tamisemi ambae pia ni mratibu msaidizi wa zoezi hilo amesema malalamiko yaliyotolewa wameyapokea na kuyafanyia kazi kwa kiasi kikubwa.
Nae Issa Asesisye ambaye ni mratibu msaidizi wa zoezi hilo pia , amesema wanafunzi walipewa maelekezo ya uchaguzi wa tahasusi na vyuo vya kati kutokana na upendeleo wao katika chaguzi walizofanya.
Wakitolea ufafanuzi kuhusu wanafunzi waliopangiwa shule tofauti na walizochagua wamesema wamefanya hivyo kutokana na uwezo wa wanafunzi pamoja na uwezo wa shule kupokea idadi ya wanafunzi.
Aidha wamesema zoezi hilo ni la haki na hakuna aliyeonewa na hivyo kuwataka wazazi na wanafunzi wenye malalamiko wafike katika ofisi za elimu Wilayani na Mikoani au kufika ofisi za Tamisemi kupata ufafanuzi zaidi au kupiga simu kupitia namba 0262160210 au 0735160210 bure.