Wananchi wametakiwa kutunza mazingira ili kunusuru kizazi cha sasa na baadae
4 June 2021, 1:36 pm
Na; Shani Nicolous.
Kuelekea kilele cha siku ya mazingira Duniani wananchi wametakiwa kuzingatia utunzaji wa mazingira ili kunusuru kizazi cha sasa na baadae.
Wito huo umetolewa na mdau wa utunzaji wa mazingira kutoka kampuni ya Vilidium Tanzania ambao ni watengenezaji wa nishati mbadala Bw. Abuu Habibu, pamoja na Bakari Mtembo kutoka asasi ya HUDEFO wakati wakizungumza na Dodoma fm hii leo.
Bw. Bakari amesema kuwa hakuna maisha bila mazingira hivyo ni vizuri kuzingatia utunzaji wa mazingira ukijumuisha upandaji wa miti pamoja na kutoa ushirikiano kwa vikundi vinavyojihusisha na ulinzi wa mazingira.
Kwa upande wake Bw.Abuu Habibu amesema kuwa ni vyema baadhi ya taasisi kutambua umuhimu wa elimu za mazingira na nishati mbadala zitakazopunguza uharibifu wa mazingira .
Ameongeza kuwa changamoto wanazokutana nazo ni kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa taasisi ili kutoa nafasi ya kampuni hizo kutoa elimu kwa uma.
Maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani hufanyika Juni 5 kila mwaka na mwaka huu imebeba kauli mbiu isemayo” tutumie nishati mbadala kuongoa mifumo ikolojia.”