Maafisa mazingira wametakiwa kuhakikisha sheria ya mazingira inazingatiwa
3 June 2021, 12:35 pm
Na; Mariam Matundu.
WAZIRI wa nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Selemani Jafo amewataka maafisa Mazingira katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 inasimamiwa katika maeneo yao.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Waziri Jaffo wakati wa ufunguzi wa semina ya maafisa Mazingira wilaya ambapo amesema suala zima la utunzaji wa Mazingira ni ajenda muhimu ambayo maafisa hao wanapaswa kuisimamia ili iweze kutekelezeka.
Amesema ajenda ya mazingira ni muhimu na dunia inataabika na uharibifu wa mazingira ikiwemo uharibifu wa misitu ya asili na ya kupanda ambayo inachomwa moto na hivyo kusababisha hali ya mazingira kuwa mbaya.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Dkt Festo Dugange ametoa maelekezo kwa Mamlaka za mitaa na sekretarieti za Mikoa kuifanya ajenda ya utunzaji wa mazingira kuwa ya kila siku.
Awali,Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Marry Maganga amesema semina hiyo ina lengo la kujadili na kutoa mapendekezo katika changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kwenye maeneo yao na kuzipatia ufumbuzi.