Halmashauri zaagizwa kupanda miti Milioni moja na laki tano
29 May 2021, 3:29 pm
Na; Mindi Joseph.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh.Seleman Jafo ameziagiza Halmshauri zote nchini kupanda miti isiyopungua Milioni moja na laki tano kila mwaka ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Jafo ametoa maagizo hayo leo jijini Dodoma wakati wa zoezi la upandaji miti kwenye eneo la Medeli lilipo jijini hapa, ambapo amesema hivi sasa hali ya hewa imebadilika katika maeneo mbalimbali kutokana na uharibifu wa mazingira huku maeneo mengine yakiwa ni makame.
Aidha, Waziri Jafo amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wameanzisha kampeni kabambe ya Usafi na Utunzaji wa Mazingira ili kukabiliana na mabadiliko hayo.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amesema kwenye ajenda ya Mkoa ni kuhakikisha kuwa Mazingira yanakuwa ya kijani na kwa kushirikiana na wadau atalisimamia hilo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Antony Peter Mavunde amesema kutokana na hali ya hewa ya Dodoma inahitaji muamko mkubwa wa upandaji miti huku akiahidi kuwa kampeni hiyo inafanikiwa kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.
Hatahivyo, kampeni hiyo ambayo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataizindua June 5 kwenye kilele cha siku ya mazingira Duniani, Waziri Jafo aliteua Wajumbe 14 washauri pamoja na mabalozi 40 wa kampeni ya mazingira yenye lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi shindani Duniani katika utunzaji wa mazingira.