Vijana Dodoma wazitaka taasisi za maendeleo kuwapa elimu
21 May 2021, 12:15 pm
Na; Thadey Tesha
Vijana jijini Dodoma wamezitaka taasisi za maendeleo ya vijana kuwapa elimu na kuwahamasisha kuchukua mkopo wa asilimia mbili unaotolewa na Halmashauri kwa ajili ya kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Wakizungumza na Dodoma fm vijana hao wamesema wanashindwa kunufaika na fungu linalotengwa kwa ajili yao kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya matumizi ya fedha hizo hivyo kuhofia kushindwa kuzirejesha.
Kwa upande wake mratibu wa shirika linalojihusisha na maendeleo ya vijana katika nyanja za kijamii na kiuchumi Restless development Bw.Denis Smel amesema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa vijana na tayari wameandaa mpango kazi wa kuwapa elimu katika suala la mikopo.
Aidha amewataka viongozi wa Mitaa pamoja na Vijiji kushirikiana na taasisi pamoja na mashirika mbalimbali ya maendeleo ya vijana ili kuleta matokeo chanya kutokana na taasisi hizo kuwa karibu nao.
Serikali imeahidi kuendelea kutoa mkopo wa asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya kukopesha vikundi vya Wanawake, Vijana Na Watu Wenye Ulemavu katika mwaka wa fedha 2021/2021