Wakazi wa lugala watanufaika na elimu ya watu wazima
7 May 2021, 11:39 am
Na; Alfred Bulahya.
Wakazi wa mtaa wa Lugala kata ya Mbalawala watanufaika na elimu ya watu wazima baada ya uongozi wa eneo hilo pamoja na wananchi kukubaliana kuanzisha darasa ili kuwasaidia wananchi ambao hawakubahatika kusoma.
Akizungumza na Taswira ya habari mwenyekiti wa mtaa huo bw. Zefania Mgutwa amesema kupitia vikao na wananchi hao wamekubaliana kuanzisha darasa hilo kwa lengo la kuongeza uelewa kwa wakazi hao.
Amesema hatua hiyo imeungwa mkono kwa asilimia kubwa na wananchi wa eneo hilo kwani hadi sasa tayari zaidi ya wananchi 80 wameandikishwa huku wananchi arobaini (40) tayari wameanza kuhudhuria masomo.
Wamesema endapo muitikio wa watu kujifunza utakua mkubwa wanampango wa kumueleza Afisa Elimu wa msingi ili aweze kuzindua darasa hilo hali itakayo ongeza hamasa kwa wananchi kujiunga na masomo hayo.
Nao wakazi wa mtaa huo wameushukuru uongozi wa eneo hilo na wamesema wapo tayari kujiunga na kuwahamasisha wananchi wengine wasione aibu wajiunge ili waweze kujua kusoma na kuandika.
Mtaa wa Lugala ni mtaa ulioko katika kata ya Mbalawala jijini Dodoma ni mtaa unao jitahidi kutatua changamoto za wananchi wake .