Dodoma FM

Kizota wauomba uongozi wa mtaa ruhusa ya kufanya usafi katika mazingira yanayo zunguka makazi yao

6 May 2021, 1:38 pm

Na; FREDY CHETI.

Wananchi wa Mtaa wa Salama Kata ya Kizota wameuomba uongozi wao kuwaruhusu kufanya usafi katika mazingira yanayozunguka makazi yao badala ya maeneo ya wazi kila ifikapo mwisho wa mwezi kama utaratibu ulivyowekwa na Serikali .

Wakizungumza na Taswira ya habari baadhi ya wananchi hao wamesema  kumekuwepo na uzito kwa wananchi kutoka kufanya usafi katika maeneo ya wazi hivyo ni vyema serikali za mitaa zikaweka utaratibu mpya ili kutoa fursa  kushiriki kwa wingi.

Aidha wamesema kuwa sheria pamoja na tozo ambazo zinambana mwananchi ambae hashiriki  kikamilifu  katika usafi ni vyema zikawa wazi ili kila mwananchi aweze kuzielewa.

Kwa upande wake Afisa mazingira wa jiji la Dodoma Bw. Dickson Kimaro amesema sheria inaelekeza wananchi kushiriki kufanya usafi kwa pamoja pia kila mwananchi ni lazima afanye usafi mita tano kuzunguka makazi yake au eneo la biashara.

Akijibu suala la wananchi kutofahamu sheria pamoja na tozo Bw. Kimaro amesema kuwa si kweli kwamba wananchi hawafahamu sheria hizo kwani wamekua wakipita mitani kutangaza na gari la matangazo  kuhusu faini pamoja na adhabu zitakazotolewa kwa wananchi ambao hawatoshiriki usafi.

Usafi wa mazingira unachangia kuwa na mazingira bora na mazingira endelevu pia  ni njia ya kuendeleza afya kwa kuzuia mawasiliano ya binadamu na athari za taka. Athari hizo zinaweza kuuhusu mwili, mikrobiolojia, biolojia au kemikali vikolezo vya magonjwa.