NGOs zatakiwa kusimamia miradi inayo lenga kuwasaidia wananchi
4 May 2021, 11:51 am
Na; Mariamu Matundu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis ameyaagiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini kuhakikisha miradi yanayoisimamia inalenga kuwasaidia wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo Wilayani Arumeru Mkoani Arusha alipotembelea mradi wa Shamba Darasa unaoendeshwa na Shirika Best Agriculture Pratice (BAP) aliokwenda kuona namna Shirika hilo linavyotoa elimu ya Kilimo cha kisasa kwa Wananchi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuendelea kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo wanayofanyia kazi.
Amesema NGOs zina mchango mkubwa sana katika jamii hasa kuwawezesha makundi maalum kujikwamua kiuchumi haswa wanawake ambao wana jukumu kubwa la kulea familia na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga amezitaka NGOs nchini ziendelee kufanya kazi kwa tija zaidi ili ziweze kusaidia wananchi kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mkuu wa Shirika la Best Agriculture Pratice Nicodemas Mabula amesema kuwa Shirika lake litatekeleza agizo la Naibu Waziri kwa kuendelea kutoa elimu ya kilimo bora kwa wananchi ili waweze kulima kwa tija na kujikwamua kiuchumi.