Dodoma FM
Dodoma FM
12 February 2026, 3:57 pm

Zoezi hilo limeandaliwa na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma likiwa na lengo la kufikia makundi yote ya wazee, watoto na kaya zenye kipato cha chini.
Na Mariam Kasawa.
Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kila mtanzania anapata fursa ya matibabu bila kikwazo cha kipato.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri wakati wa zoezi la ugawaji wa kadi za bima ya afya kwa kaya maskini zoezi lililofanyika katika Kata ya Nala.
Alisema kuwa Bima ya Afya ni mkombozi wa matibabu kwa kaya zisizo na uwezo.
Aidha, aliwahimiza wananchi waliojitokeza kwa wingi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa wote ili kujihakikishia huduma bora za matibabu na kupunguza adha ya gharama kubwa wanapougua.
Nae, Mwananchi wa Kata ya Nala, Samweli Mkonongo aliishukuru serikali kwa hatua hiyo, akieleza kuwa itawasaidia kupata matibabu kwa wakati na kuondoa utegemezi wa kuchangishana fedha wanapopatwa na maradhi.