Dodoma FM
Dodoma FM
27 January 2026, 5:16 pm

Aidha, ilielezwa kuwa eneo la Engusero Andare lilitengwa mahsusi kwa ajili ya jamii ya Wandorobo, ambao maisha yao yanategemea zaidi shughuli za asili ikiwemo uvunaji wa asali kama chakula chao kikuu.
Na Kitana Hamis.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, amewaagiza wananchi waliovamia eneo la Engusero Andare lililopo Kijiji cha Kimana, Wilaya ya Kiteto, kuondoka mara moja katika eneo hilo lenye ukubwa wa takribani ekari 4,000.
Akizungumza na wananchi wa Engusero Andare alipofika kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu, Mheshimiwa Sendiga alisema uvamizi wa eneo hilo ni kinyume cha sheria, kwani eneo hilo limetengwa rasmi kwa ajili ya makazi na malisho ya jamii ya Wandorobo wanaoishi porini.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wananchi waliovamia eneo hilo wamekuwa wakifanya shughuli za kilimo katika eneo ambalo haliruhusiwi kwa matumizi hayo, ambapo hadi sasa takribani ekari 3,000 zimeharibiwa na kulishwa.
Katika hatua ya kudhibiti mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto ameunda kamati maalum ya kutatua mgogoro wa ardhi, huku Mkuu wa Mkoa akisisitiza msimamo wa Serikali wa kulinda haki za jamii husika na matumizi sahihi ya ardhi.