Dodoma FM
Dodoma FM
23 January 2026, 2:26 pm

Hatua hiyo inajiri ikiwa ni siku ya pili tangu Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuzindua rasmi zoezi la ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum, zoezi inalotekelezwa ikiwa ni sehemu ya sera ya serikali kuhakikisha watoto wote wanajumuishwa katika mfumo wa elimu bila ubaguzi.
Na Lilian Leopold.
Zaidi ya watoto 22 wenye mahitaji maalum wamebainishwa katika kata ya Kizota, jijini Dodoma, huku wito ukitolewa kwa wazazi na walezi kuacha kuwaficha watoto hao na badala yake kushirikiana na serikali ili waweze kupata haki zao za msingi kama elimu.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Afisa Elimu kata ya Kizota Robert Tesha amesema zoezi hilo limekwenda vizuri, huku wazazi wakijitokeza kuwaleta watoto wao.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji kata ya Kizota, Aidani Levananga amesema ubainishaji wa watoto umefanyika kwa kupita mitaa mbalimbai ya kata hiyo kwa ushirikiano wa karibu na viongozi wa serikali za mitaa.

Shida Matonya, mkazi wa mtaa wa Area A na ni mzazi wa mtoto mwenye mahitaji maalum amesema ameridhishwa na zoezi hilo akieleza kuwa inatoa matumaini mapya kwa watoto wenye changamoto mbalimbali.
Kwa ujumla, zoezi la ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum linaelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wa kutekeleza elimu jumuishi na kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma, huku matarajio yakiwa ni kuwafikia watoto wengi zaidi katika kata na mitaa ili kuwajumuisha rasmi katika mifumo ya elimu na huduma za kijamii.