Dodoma FM
Dodoma FM
23 January 2026, 11:04 am

Picha ni wadau wa afya katika utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa vituo vya afya katika mikoa ya kanda ya kati. Picha na Wizara ya Afya.
Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma kwa makundi maalum kama akina mama, watoto na wazee, pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma bora na salama kwa wananchi kwa ujumla.
Na Victor Chigwada.
Wananchi wa kijiji cha Msanga, wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma za afya, hususan kupitia ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika zahanati ya kijiji hicho.
Wananchi wamesema hatua hiyo imeondoa changamoto kubwa iliyokuwepo awali ya kuchanganya wagonjwa wa kawaida na mama wajawazito kutokana na ukosefu wa miundombinu maalum.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Msanga, Hatibu Ally, amesema ujenzi wa jengo la mama na mtoto ni sehemu ya safari ya maboresho ya zahanati hiyo, huku kukiwa na mipango ya muda mrefu ya kuipandisha hadhi na kuwa kituo cha afya ili kuwahudumia wananchi wengi zaidi.
Ameongeza kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto ndogondogo ikiwemo uhaba wa baadhi ya watumishi na huduma, uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na wataalamu wa afya umeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha utoaji wa huduma, hususan kwa makundi maalum kama wazee na akina mama.