Dodoma FM

Askofu Kingamkono awahimiza waumini kutenda mema

23 January 2026, 9:55 am

Picha ni baadhi ya waombolezaji waliojitokeza katika mazishi ya aliyekuwa Meya wa Jiji la Dodoma Francis Mazanda katika Kanisa la Watakatifu Wote lililopo Kata ya Vig’hawe, Wilaya ya Mpwapwa. Picha na Steven Noel.

Miongoni mwa waliotoa salamu za rambirambi ni pamoja na Ezekia Chibulenje, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chilonwa, pamoja na George Malima Lubeleje, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, ambao kwa pamoja wamesema marehemu alijipambanua kwa maadili mema, uwajibikaji na uongozi uliotanguliza maslahi ya wananchi.

Na Steven Noel.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa, Mhashamu Luznet Kingamkono, amewataka waumini wa kanisa hilo pamoja na jamii kwa ujumla kutojisahau kutenda mema, akisisitiza kuwa kifo huja bila taarifa, hivyo kila mmoja anatakiwa kuishi kwa kumcha Mungu na kutenda haki wakati wote wa uhai wake.

Askofu Kingamkono ametoa wito huo wakati wa ibada ya mazishi ya aliyekuwa Meya wa Jiji la Dodoma katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2005, iliyofanyika katika Kanisa la Watakatifu Wote lililopo Kata ya Vig’hawe, Wilaya ya Mpwapwa.

Katika mahubiri yake, Askofu Kingamkono amesema kuwa mara nyingi watu wanapofanikiwa kibiashara au kupanda ngazi za uongozi, humsahau Mungu na kuanza kutegemea vyeo, mali au kazi, hali inayowafanya kupuuzia ibada na misingi ya imani.

Ameongeza kuwa maisha ya mwanadamu ni ya muda mfupi, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kuishi kwa kutenda mema, kuzingatia haki na kudumisha uhusiano mzuri na Mungu pamoja na wanadamu wenzao.

Picha ni baadhi ya waombolezaji waliojitokeza katika mazishi ya aliyekuwa Meya wa Jiji la Dodoma Francis Mazanda . Picha na Steven Noel.

Wakizungumza kuhusu maisha ya marehemu, baadhi ya waombolezajiwameeleza kuwa alikuwamtu wa ukweli, uaminifu na mwenye kujitolea katika utumishi wa umma pamoja na shughuli za kanisa.

Ibada ya mazishi imefanyika katika Kanisa la Watakatifu Wote Vig’hawe, huku mazishi yakifanyika katika Makaburi ya Vig’hawe, eneo la Namba 30, Wilaya ya Mpwapwa.

Sauti ya Steven Noel.